Search This Blog

Sunday, May 18, 2014

LIMAO NA NDIMU


Ni matumaini yangu kuwa hujambo.

   Limao na ndimu ni vitu tunavyotumia mara kwa mara katika mapishi, na inaonekana kama ni vitu vidogo vya kuongeza ladha katika chakula. Ukweli ni kwamba limao/ ndimu ni matunda madogo kwa umbo lakini yana matumizi mengi na faida nyingi tu.  Basi leo nimeona si mbaya ni kaongelea  machache  kuhusu uchaguaji, utumiaji, utunzaji na faida zake.
  Kwanza kabisa ukienda kununua chagua ndimu/limao kubwa yenye ngozi laini na nyembamba  ( usichukue yenye ngozi ngumu) na yenye rangi iliyokolea vizuri hiyo huwa fresh na ina kuwa na maji mengi. Changua ndimu/limao iliyo katika hali nzuri ambayo haijaanza kuharibika.
Limao na ndimu mimi huwa nazitumia kwa matumizi yafuatayo,
   Maji moto yaliyochanganwa na ndimu, ni nzuri kunywa kila asubuhi hasa kwa watu wanaotaka kupunguza uzito, kabla ya kula chochote  tafiti zinaonyesha watu wanaotumia sana ndimu/limao kwenye diet zao wana uwezakano mkubwa wa kupunguza uzito kuliko wengine. Pia kwa watu wenye tatizo la harufu mdomoni ukinywa inasaidia kupunguza harufu mbaya mdomoni na kuondoa hangover.
Chemsha maji ya moto, weka katika kikombe kamulia ndimu/limao nusu inakuwa tayari kwa kunywa unaweza kuongeza asali kijiko kimoja cha chai ukipenda.

 
Lemonade, au unaweza kuiita juisi ya limao ni kinywaji kizuri sana mi nakitumia mara kwa mara na imenisaidia kuachana na soda. Juisi ya limao ni nzuri inasaidia usagishaji wa chakula mwilini na kutuliza matatizo ya kiungulia na kubakua. Pia inarahisisha mfumo wa utajoaji taka mwilini kufanya kazi vizuri. Juisi ya limao unatengeneza kama juisi ya chungwa, ila weka sukari kidogo sana.
 

 Kila mtu anajua umuhimu wa kunywa maji mengi, mimi katika kujitahidi kuyafanya maji yangu yavutie na yawe na ladha huwa naweka kipande cha ndimu/limao ndani ya maji.

Natumia ndimu/limao kwenye nyama, samaki na salad au kachumbari kuongeza ladha, kupunguza mafuta kwenye nyama na kutoka shombo kwenye samaki.
Pia natumia ndimu na limao kuweka harufu nzuri kwenye fridge na microwave. 
Fridge, chukua pamba weka katika kisahani cha chai halafu kamulia ndimu/limao weka katika fridge kwa saa kadhaa kisha toa itafanya fridge yako isiwe na harufu zisizoeleweka.
Microwave, chukua kibakuli jaza maji kiasi weka kipande cha ndimu kwenye bakuli ingiza kwenye microwave na iwashe kwa dakika kama tatu, kisha toa kama kuna mvuke kausha kwa kitambaa kikavu, na microwave itakuwa katika harufu nzuri.


Limao/ndimu unaweza kuhifadhi jikoni sehemu iliyo kavu na hewa hata kwa wiki moja, ila ukitaka ikae zaidi zifunge kwenye mfumo wa plastic na weka katika fridge, zitakaa zaidi ya siku kumi.
Angalizo, watu wanasema si vizuri kuwapa watoto chini ya miaka 10 vitu vya limao na ndimu mara mara, sijajua bado sababu ni ipi, ila si mbaya ukizingatia.
 Haya  ni hayo tu kwa leo, unakaribishwa kuchangia chochote kile kuhusu limao na ndimu, karibu.